Elimu ya FedhaUncategorized

Jinsi ya Kukopesheka na Taasisi za Fedha

Ndugu mfuatiliaji wa makala zetu, leo napenda tujadili jinsi unavyoweza kuaminiwa na kukopa fedha kwenye taasisi zinazotoa mikopo.

Moja ya changamoto zinazowakumba watu wengi ni kushindwa kukubaliwa mikopo na taasisi za kifedha. Hali hii mara nyingi si kwa sababu hawastahili kupata msaada, bali kwa sababu hawajatimiza vigezo vinavyofanya mtu kuwa kukopesheka.

Kwanza kabisa, taasisi za kifedha huangalia historia yako ya kifedha. Ikiwa umewahi kukopa na hujalipa kwa wakati au hujalipa kabisa, taasisi nyingi zitakuwa na wasiwasi kukukopesha tena. Ni muhimu kuwa na rekodi nzuri ya ulipaji, hata kama ni mikopo midogo.

Pili, uwezo wako wa kurejesha ndiyo kipimo kikubwa cha kuaminiwa. Taasisi huangalia kipato chako cha kila mwezi na matumizi yako ya msingi ili kuhakikisha unaweza kurejesha mkopo bila kuathiri maisha yako ya kila siku. Hii ndiyo maana taarifa kama salary slip, business receipts au mikataba ya ajira ni muhimu unapowasilisha maombi.

Tatu, nidhamu ya kifedha inaonyesha tabia yako na utayari wa kuwa na uwajibikaji. Mtu ambaye anajitunza kipesa, ana akaunti benki inayotumika, na anajiwekea akiba mara kwa mara, huaminika zaidi.

Nne, taasisi nyingi huangalia mali au dhamana inayoweza kutumika kama kinga ya mkopo. Hii si lazima kwa kila mkopo, lakini ni kigezo kinachoongeza nafasi zako, hasa kwa mikopo ya muda mrefu au yenye kiasi kikubwa.

Mwisho, kuwa na mawasiliano mazuri na uaminifu wakati wa kujaza fomu au kuhojiwa ni muhimu sana. Usifiche taarifa. Toa kila kitu kwa uhalisia, kwani uwazi hujenga uaminifu na huchochea mafanikio ya maombi yako.

Kwa ujumla, kukopesheka si bahati ni matokeo ya maandalizi, uwajibikaji na tabia bora ya kifedha. Hapa CF Microcredit, tunahimiza wateja wetu kuwa tayari kabla ya kuomba mkopo, ili kuhakikisha wanapata suluhisho sahihi na la kudumu kwa maendeleo yao ya kiuchumi.

Endelea kujifunza na unufaike na makala zetu za elimu na ushauri wa kifehda.

Mwandishi: Habel Samida | @habelsamida

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!