Elimu ya FedhaUncategorized

Mbinu 10 za Kutoka Kwenye Umasikini (Sehemu ya 5)

Karibu mpenzi mfuatiliaji wa makala zetu. Hii ni sehemu ya tano, katika mwendelezo wa makala ya Mbinu 10 za Kutoka kwenye Umasikini. Awali ya yote, kabla hujaendelea natamani uende ukasome sehemu ya kwanza, pili ya 3 pamoja na ile ya nne kwakuwa zimebeba msingi wa kuelewa sehemu hii ya tano.

Katika sehemu zilizopita, tulijifunza kuhusiana na dhana ya utajiri na umasikini na uhusiano wake na fikra za mwanadamu. Kwahiyo, utajiri ni matokeo! Kama ulivyo umasikini. Hiyo inatupa picha kwamba, mtu yeyote anaweza kubadilisha matokeo kwa kuelewa na kufuata kanuni ambazo zimethibitishwa na kutumiwa na watu wengi ambao wamefanikiwa.

Pamoja na hayo, tulijifunza mbinu kadhaa. Mbinu ya kwanza; Tafuta kuwa na kipato endelevu, Pili, Kuweka akiba. Tatu, Ishi chini ya kipato chako, nne, ongeza kipato chako. na mbinu ya tano ambayo ni kutumia taasisi za kifedha ili kukuwezesha kukua kwa haraka zaidi ya kudunduliza kipato chako kidogo kidogo. Leo tunaendelea na mbinu ya sita naya saba ambazo ni kuepuka madeni yasiyo na tija. Pamoja na kulinda mbegu yako isipotee. Twende sasa tujifunze.

Mbinu ya Sita.
Epuka Madeni Yasiyo na Tija.

Madeni ni mtego wa kifedha unaowakaba watu wengi bila wao kujua. Ukiona mtu amejitahidi kujenga kipato, akaweka akiba, akalinda mbegu yake, lakini bado hana amani ya kifedha—tatizo mara nyingi ni madeni. Tatizo siyo deni lenyewe, bali aina ya deni analochukua.

Kuna madeni ya kizembe – yale ya kuendesha maisha ya starehe zisizohitajika: simu mpya kila mwaka, nguo za kifahari, sherehe kubwa za kuonesha uwezo. Haya madeni hayazai kitu, bali yanakula kile ulichokuwa umejenga. Ni sawa na kuchukua mbegu na kuila badala ya kuipanda.

Lakini pia kuna madeni yenye tija – yale yanayotumika kuwekeza kwenye mradi au chombo kinachozalisha kipato zaidi ya riba ya deni lenyewe. Hii ndiyo aina pekee ya deni linalokubalika, na hata hivyo, linahitaji umakini mkubwa na hesabu sahihi kabla ya kuingia.

Tatizo ni kwamba wengi huingia kwenye madeni bila mpango, wakiendeshwa na tamaa au shinikizo la kijamii. Matokeo yake, kipato chote wanachopata kinamalizika kwenye marejesho ya mikopo na riba, wakibaki maskini licha ya kufanya kazi kwa bidii.

Unapaswa kujifunza kuwa huru na madeni yasiyo na tija. Usikimbilie mkopo kwa kila tatizo dogo. Fanya mazoea ya kupanga na kutunza akiba, ili unapokutana na changamoto usikimbilie kukopa. Deni liko kama kifaa cha moto: likitumika vibaya linachoma, lakini likitumika kwa akili linaweza kukupikia chakula kitamu.

Mwisho wa siku, uhuru wa kifedha unapatikana pale ambapo kipato chako si mali ya benki au mabaashara, bali kinabaki mikononi mwako kukusaidia kufanikisha ndoto zako.

Mbinu ya Saba
Linda Mbegu Yako Isipotee.

Hii ndiyo hatua inayotenganisha washindi na waliopoteza kila kitu walichokijenga. Umejinyima kwa muda mrefu, umeweka akiba kila mwezi, na sasa umekusanya hazina inayoweza kubadilisha maisha yako. Lakini kumbuka, hii si fedha ya kawaida ya matumizi ya kila siku – hii ndiyo mbegu yako. Na mbegu ikiharibika, hakuna mavuno tena.

Tatizo kubwa la watu wengi ni tamaa ya haraka. Wanaposhika mtaji mkononi, mara moja wanakurupuka kuwekeza kwenye miradi ambayo haijathibitishwa, wakiahidiwa faida kubwa ndani ya muda mfupi. Ni sawa na mkulima anayepanda mbegu kwenye udongo usio na rutuba, kisha ashangaa kwanini hakuvuna.

Unapaswa kulinda akiba yako kwa akili na hekima kubwa. Usiweke kila kitu kwenye mradi mmoja usio na historia ya mafanikio. Usiwaamini watu bila kujua rekodi yao ya uaminifu na uwezo. Na zaidi ya yote, usiwekeze kwa kusukumwa na hisia au presha za marafiki na ndugu. Fedha haijui undugu, haijui urafiki – ni sheria moja tu, ikipotea imetoka.

Chukulia mfano wa watu waliowekeza pensheni zao kwenye miradi isiyokuwa na uhalisia, wakiahidiwa faida mara mbili ndani ya miezi michache. Matokeo yake walipoteza kila kitu walichokuwa wamejenga kwa miaka mingi ya jasho na machozi.

Mbegu hii uliyoikusanya ni ya thamani kubwa mno. Ilinde kama unavyolinda moyo wako. Kabla ya kuwekeza, fanya utafiti, tafuta ushauri wa kitaalamu, na hakikisha mradi au biashara unayoingia ina msingi imara. Hii ndiyo njia pekee ya kuhakikisha mbegu yako inaleta mavuno makubwa badala ya kukauka kabla haijachipua

Tukutane sehemu inayofuata. Asante kwa kufuatilia makala zetu kwa ajili ya kujifunza elimu ya fedha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!