Mbinu 10 za kukutoa kwenye Umasikini (Sehemu ya 1)
Umasikini, kama ullivyo utajiri ni matokeo! Kama hali hizo ni matokeo, basi tambua kuwa kuna chanzo. Chanzo ni mambo au mipango na hatua za kufuata ili kufikia. Unaweza kuniuliza, “Habel, kuna mtu yeyote anaye chagua umasikini au anayeweka mipango ili awe masikini? Jibu lipo kwenye makala hii. Kadri unavyosoma, utagundua jawabu sahihi kama watu waachagua matokeo ya umasikini au la!
Miaka mingi kidogo imepita, wakati nipo kidato cha kwanza, ilikuwa siku nzuri ya kutukaribisha kidato cha kwanza shuleni hapo. Mgeni rasmi alikuwa mmoja wa viongozi wa taasisi moja kubwa ya dini lakini pia alikuwa na nafasi ya mjumbe wa bodi wa kamati ya shule. Siku hiyo, aliongea maneno ambayo yamebaki kwenye medula zangu hadi leo, na sitegemei kuyasahau kwa kipindi chote nitakachokuwa naishi hapa duniani.
Alisema….”Maendeleo au ufukara, vyote husababishwa na mfumo wa fikra za watu” Maneno hayo yaliibua maswali mengi kichwani mwangu zaidi ya majibu. Nilianza kujiuliza; “inawezekaneje mtu achague fikra za umasikin?” Nilihusisha na hali ya familia yangu ambayo ilikuwa ikiishi kwenye umasikini, nilipiga picha ya jamii kwa ujumla iliyokuwa katika mazingira yale, ikiwa imezingirwa na umasikini kwa kiasi kikubwa.
Huo ulikuwa mwanzo wa kuanza kufikiri. Kufikiri namna ambavyo fikra zina mahusiano ya moja kwa moja na umasikini au utajiri. Ilikuwa ni cheche ya moto ambayo ilianza kulipua adhma ya kujifunza, kudadisi na kutamani kujua kwa undani kwakuwa sikuufurahia umasikini. Niliona, kama kuna namna nzuri ya kufikiri, ni vyema niijue ili jamii yangu itoke kweye lindi la umasikini.
Miaka mingi baadaye, nimekuwa mwalimu, muhamasishaji na msahauri wa mambo ya uchumi binafsi, kazi, biashara na mambo mbalimbali ya maisha kupitia kujifunza na kuzitumia mbinu mbalimbali ambazo nimeziweka pamoja na kuandika siyo tu makala kama hii unayosoma, bali vitabu ambavyo vimegusa maisha ya watu kwa namna chanya.
Kabla sijazungumzia mbinu 10 za kukutoa kwenye umasikini, nataka tujifunze kidogo kuhusu FIKRA na namna zinavyoweza kuleta matokeo ya aidha maendeleo au kudumaa kimaendeleo. Sayansi na saikolojia zimeonesha tafiti kuwa; mtazamo wa mtu unaathiri sana matokeo yake ya maisha. Watu wenye fikra chanya na ya ukuaji mara nyingi huona changamoto kama fursa, hujitahidi kujifunza kutokana na makosa, na hivyo kufanikiwa kimaendeleo.
Kwa upande mwingine, mtu mwenye fikra hasi au ya ukomo mara nyingi huona vizuizi vinavyomzunguka kama barabara zilizofungwa, jambo linalosababisha kushuka kwa motisha, ujasiri, na kufikia malengo. Hali hii mara nyingi inalingana na matokeo duni kimaisha, kifedha, au kitaaluma.
Neurobiolojia pia inaonyesha kuwa mtazamo chanya husaidia kuboresha ufanisi wa ubongo, kuongeza ubunifu, na kuongeza uwezo wa kushughulikia msongo wa mawazo. Kwa upande mwingine, mtazamo hasi unaweza kusababisha msongo mkubwa, wasiwasi, na uharibifu wa afya ya akili, jambo linalopunguza uwezo wa kufanya maamuzi yenye busara.

Kwa kifupi, jinsi mtu anavyofikiria si tu inaathiri hisia zake, bali pia huunda mwelekeo wa maisha yake. Kubadilisha mtazamo kuwa chanya na wa ukuaji ni njia yenye nguvu ya kuongeza uwezekano wa kufanikisha malengo na kujenga maisha yenye tija na mafanikio.
Fikra zetu haziji tupu; zinatokana na ubongo na akili chini ya fahamu (subconscious mind), ambapo mawazo, uzoefu, na yale tunayoyasikia au kuona hujengwa na kuhifadhiwa kama “programs” zinazotawala jinsi tunavyoshughulikia maisha. Kila ujumbe, tabia, au picha tunayokutana nayo mara nyingi huacha alama ndani ya akili yetu, ikiunda mtazamo wa wa namna tunavyiona dunia.
Mambo haya siyo sayansi ngumu ya kurusha roketi angani! Nitajitahidi kutumia lugha rahisi zaidi ambayo utaielewa kwa haraka na urahisi. Tuchukulie mfano wa tanki kubwa la maji, hilo tulipe mfano wa kichwa chako! Ambapo, katika hili tanki unamimina maji.
Ikiwa unamjaza majitaka kwenye tanki, unatarajia ukifungua bomba la tanki hili utapata maji safi? Ndivyo ilivyo kwenye mfumo wa akili yako. Mambo ambayo unayajaza kichwani au akilini ndiyo yanajenga mtazamo au fikra juu ya maisha. Kama maneno unayosikia kila siku ni hasi, ya kukatisha tamaa au lawama, matusi na uongo! Ndiyo yatakayoijaza akili yako. Matokeo yake, ukifungua kinywa utaongea yale yaliyoijaza akili yako.
Akili hukusanya jumla ya mambo yote unayo jifunza, kuyaona au kuyasikia na kuyatunza kama mafaili kwenye akili yako sehemu ambapo hutunza kumbukumbu. Ikitunzwa kama kumbukumbu, hizo ndizo zitakuwa taarifa zinazoongoza masha yako na kuathiri maamuzi na kukufanya uwe na aina ya maisha ambayo yanawiana na aina ya taarifa iliyo kichwani mwako.
Kwahiyo, ili uweze kutawala fikra zako na kujenga mtazamo chanya, utakao kujenga na kukuinua kuelekea kwenye maendeleo, uthubutu na nidhamu unapaswa kufanya jitihada za makusudi kutawala kila taarifa inayopita akilini mwako. Hii ni kuanzia aina ya marafiki au watu unaokuwa nao mara nyingi. Jiulize aina ya mazungumzo yao yakoje? Kama ni “unatembea na mwizi” basi nawe utakuwa “mwizi” kama ambavyo msemo wa wahenga unasema.
Jifunze, ambatana na watu wanao thubutu wasio walalamikaji na kutupia lawama wengine bila kuchukua hatua na kushika hatamu za maisha yao. Jisome, epuka matumizi mabaya ya mitandao kuangalia mambo ambayo hayakujengi, badala yake tumia fursa au jukwaa hilo kujifunza ili uwe mtu bora zaidi
Hudhuria semina na mafunzo yatakayo kuongoza katika ukuaji zaidi. Weka nidhamu na mikakati madhubuti. Acha kukaa kwa kupoteza muda, fanya kazi kwa bidii, imarisha motisha ya ndani na kuweka nidhamu, utafika mbali kokote unako tarajia.
Ninapo zungumza habari hizi za fikra na mtazamo chanya haimaanishi maisha hayana changamoto, bali ikufanya kufikiria kuongeza uwezo wa kuona fursa, kushughulikia vizuizi, na kuunda njia za mafanikio hata pale mazingira yanapokuwa magumu.
Amua leo kuwa mtu wa mabadiliko, kwakuwa ukiweza katika eneo hili la muhimu, itakuwa rahisi kuzitumia mbinu 10 ninazokwenda kukueleza ambazo zinaweza kubadilisha kabisa maisha yako, na baada ya muda utafurahi kwakuwa umechukua hatua na kufanikisha maisha yenye tija zaidi.
Kuendelea sehemu ya Pili, muendelezo wa makala hii bonyeza HAPA:::::
