Elimu ya FedhaUncategorized

Mbinu 10 za kukutoa kwenye Umasikini (Sehemu ya 2)

Hatimaye tumefika sehemu ya pili ya somo letu zuri na muhimu, mbinu 10 za kukutoa kwenye umasikini. Kabla hatujaendelea, napenda kukumbusha kwa muhtasari kile tulichojifunza kwenye somo llilopita. Na kama hujasoma somo lililopita, tafadhali hakikisha unasoma kwa kubofya HAPA. Somo hilo limebeba msingi wa kuelewa na kusimamia mbinu hizi

Kwa muhtasari, somo la kwanza tulijifunza kuhusiana na uhusiano wa moja kwa moja kati ya fikra au mtazamo wako na matokeo ya maisha. Mfumo wa fikra ni jumla ya mawazo yanayojirudia mara kwa mara akilini mwako na kuunda mtazamo wa kudumu. Mara nyingi haujengeki kwa siku moja bali hutokana na kile unachosikia, unachoona na unachoruhusu kuingia kwenye akili yako kila siku.

Mifumo hii ya fikra huwa kama lenzi inayokufanya uone dunia kwa mtazamo fulani. Wapo watu ambao kila changamoto huiona kama nafasi ya kujifunza, kwa sababu mfumo wao wa fikra umejengeka kwenye matumaini na uthubutu. Vivyo hivyo, yupo ambaye kila kikwazo huona mwisho wa safari kwa sababu mfumo wake umejengeka kwenye hofu na mashaka. Hapa ndipo tunagundua kuwa maisha unayoishi leo ni picha ya mifumo ya fikra uliyoijenga kwa muda.

Sasa swali ni, tunawezaje kujenga mtazamo chanya? Jibu ni kuanza na nidhamu ya mawazo. Unapoweka mazoea ya kusoma vitabu vinavyojenga, kukaa karibu na watu wenye mitazamo ya maendeleo na kujifundisha kuzungumza maneno ya matumaini badala ya malalamiko, taratibu unaunda mfumo mpya wa fikra. Ni kweli changamoto haziepukiki, lakini namna unavyopokea na kuzitazama ndizo zitakazobadilisha matokeo yako. Kujenga mtazamo chanya pia kunahitaji kushukuru kwa yale madogo uliyonayo, kwa sababu shukrani huipanua akili kuona fursa badala ya vikwazo. Kumbuka, mfumo wa fikra chanya sio hali ya kuzaliwa nayo bali ni zao la mazoea na maamuzi ya kila siku. Ukianza kulilea leo, kesho yako itabeba matokeo tofauti kabisa.

Mbinu 10 za kutoka kwenye umasikini
Mbinu ni hatua za kimkakati zinazotumika kutatua changamoto fulani au kufanikisha jambo. Kwa muktadha huu, tunaposema mbinu za kutoka kwenye umasikini tunazungumzia mikakati au njia mahsusi ambazo mtu anaweza kuzitumia kujinasua kutoka hali ya kutokuwa na kipato cha kutosha, hali ya utegemezi au mazingira ya kudumu katika maisha ya dhiki.

Mbinu huja na ramani ya njia nzima ya namna ya kujiokoa na janga la umasikini. Ndiyo maana kila uwanja wa maisha, mbinu huwa silaha kubwa ya ushindi. Mwanafunzi anapokuwa na mbinu bora za kujisomea, anapata matokeo ya ufaulu. Mfanyabiashara akitumia mbinu sahihi za kuuza na kudhibiti fedha, biashara yake inakua. Viongozi wa taasisi wanapotumia mbinu bora za uongozi, taasisi zao hupiga hatua. Kwa hiyo, maisha bila mbinu hubaki kugota, lakini maisha yenye mbinu hubeba ushindi.

Hapa nitaeleza mbinu 10 kabambe ambazo zikitumika kwa vitendo zitakutoa kimasomaso. Ninasisitiza kwenye vitendo kwa sababu kujua ni hatua moja tu, lakini kutekeleza ndiko kunakoleta matokeo. Wapo wengi wanaojua namna ya kujinusuru lakini hukwama kwa sababu hawatekelezi walichojifunza. Bill Gates aliwahi kusema: “Kuzaliwa masikini si kosa lako, lakini kufa masikini ni kosa lako.” Kauli hii inatufundisha kwamba kuzaliwa katika familia yenye changamoto za kifedha si kosa, lakini kukaa na kuridhika na umasikini hadi mwisho wa maisha ni kosa kubwa.

Sasa basi, twende moja kwa moja katika mbinu zenyewe za kutoka kwenye umasikini:

Mbinu ya kwanza; 
Tafuta kuwa na kipato endelevu cha uhakika. Hatua ya kwanza ya kujikwamua na kufikia mafanikio ya kifedha ni kuwa na kipato endelevu. Hapa kiasi haijalishi, kitu cha kwanza unachopaswa kuwa nacho ni kipato cha uhakika ambacho kitakuwa endelevu. Tafuta kitu cha kufanya. Iwe ni kazi, biashara au shughuli ambayo itakuingizia kipato. Kusema kuwa uko kwenye safari ya kuyafikia mafanikio ya kifedha wakati huna kabisa kipato ni sawa kabisa na kusubiria meli kwenye kituo cha daladala.

Zipo shughuli nyingi unaweza kufanya. Ziwe za kuajiriwa au kujiajiri. Ukiwa huna kitu, sidhani kama unaweza kubagua sana shughuli ya kufanya kwakuwa inakuingizia kipato kidogo. Kwa mtazamo wangu, unapkuwa na njaa sana karibia uzimie, hutokuwa na uchaguzi wa chakula unachotaka kula. Unaweza kula hata maharage, wakati ambapo kwa kawaida huwa huyapendi. Lakini utakaposhiba au kupoza njaa yako, unaweza kuwa na nguvu ya kukataa chakula usichopenda

Inaweza kusikitisha ukiwa kijana umemaliza chuo halafu umekaa tu mtaani unasema unatafuta kazi, wakati zinakuja nafasi za mshahara mdogo ambazo unaweza kujishikiza wakati ukitafuta zile zenye masilahi manono. Mbaya zaidi hata kujishughulisha kwenye biashara au kitu kingine hajishughulishi.

Tunapaswa kujifunza kuwa, maisha yamebadilika. Tofauti na wazazi wangu wakati wanakua. Walinisimulia kuwa; ajira zilikuwa nyingi kiasi ambacho hata wakati wanasoma kuna makampuni nataasisi ziliwafuata na kuwapa nafasi za ajira, pindi wanapomaliza tu masomo wanakwenda moja kwa moja.

Leo hii hadithi ni tofauti. Kwahiyo, inahitaji mikakati tofauti pia. Unaweza kujiajiri kwa kufanya shughuli fulani, siyo lazima iwe ya uwekezaji mkubwa wa fedha. Lakini, kama huna fedha kabisa ya kuwekeza, unaweza kufikiria kutoa huduma. Kama umesomea ujuzi fulani mfano sheria, elimu au nyingine unaweza kuitumia kutoa huduma hizo na watu wakakulipa fedha.

Kila mtu, msomi kwa asiyesoma tunahtajika kuwa na chanzo cha kipato. maish a hayaangalii kuwa wewe umesoma, hujasoma! Hata hivyo,  elimu za darasani zinaweza zisikusaidie sana kuboresha maisha yako pasipo kujiongeza na kujifunza vitu vipya vitakavyo kusaidia. Kuna watu nawafahamu, hawajafika hata shule ya sekondari. Lakini wanafanya mambo makubwa na wanajua mambo mengi kwenye biashara kwasababu waliamua kuwekeza katika kujifunza.

Anyways, nisiende mbali zaidi nisije nikatoka kabisa kwenye mada. Ninachosisitiza hapa ni kuwa na kipato. Kiasi haijalishi, ilimradi kipato kinaingia. Suala la kiasi ni lingine, lakini mafanikio huja kwa hatua na hatua ya kwanza ni hii. Mwanzo huwa ni muhimu, hata kama ni mdogo lakini ni bora zaidi kuliko kutokuanza au sifuri kabisa.

Tukutane sehemu ya 3 kwa ajili ya muendelezo…..

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!