Hilimisho: Mbinu 10 za Kutoka Kwenye Umasikini (Sehemu ya 6)
Ndugu msomaji wa makala zetu, asante kwa kufuatilia makala hizi. Huu ni muendelezo wa makala za Mbinu 10 za kutoka kwenye Umasikini. Tulianza Kuanzia mbinu ya kwanza katika sehemu ya kwanza, kisha tukaendelea na mbinu zingine kwenye sehemu zilizofuata.Kama hujasoma makala za nyumba, nakushauri uzisome, maana zinajenga msingi wa kuelewa mtiririko mzima.
Hapa tunaenda kuangalia mbinu zinazofuata katika sehemu hii ambayo ndiyo itakuwa hitimisho la mfululizo wa makala hizi. Tunategemea kuwa na makala zingine nzuri zaidi kwa ajili ya kukuelimisha kuhusiana na elimu ya fedha. Twende tujifunze mbinu zilizobakia katika kuhitimisha.
Mbinu ya nane.
Toa na Bariki Wengine.
Kuna siri kubwa kwenye ulimwengu wa fedha ambayo wengi hawaioni. Siri hii ni ya kipekee kwa sababu inaonekana kama kinyume na mantiki ya kawaida: ukitoa, unapokea zaidi. Ni kama shamba—ukihifadhi mbegu zote hutazalisha mazao, lakini unapopanda mbegu, ardhi hufunguka na kukupa mavuno makubwa zaidi.
Kuwasaidia wengine, kuchangia katika jamii au kuunga mkono misingi mizuri ya maendeleo si kupoteza, bali ni kuwekeza kwenye urithi unaodumu. Watu wanaojua kutoa, hujifunza kutazama fedha si kama kitu cha kushikilia kwa hofu, bali kama chombo cha kuleta thamani kubwa kwa wengine.
Wakati mwingine baraka za kweli haziji kwa namna tuliyotarajia. Unaweza kusaidia kijana kwa ushauri mdogo, akawa mfanyabiashara mkubwa kesho na akakuinua kuliko ulivyowahi kuota. Au unaweza kuchangia kidogo kwenye jamii, na matokeo yake ni amani na heshima ambayo huwezi kuipima kwa fedha.
Hata kwenye vitabu vya hekima za kale, imeandikwa: mkono utoao hautakosa. Hii inatufundisha kuwa sehemu ya mafanikio yetu haipo tu kwenye kulimbikiza, bali kwenye kuruhusu baraka hizo zipite na kugusa wengine.
Kwa hiyo, unapojenga utajiri, usiishie kwako tu. Toa kwa familia yako, saidia jamii yako, changia misingi ya maendeleo. Huo ndio urithi wa kweli wa kifedha na maisha—kwa sababu mwisho wa safari, sio mali utakayoacha pekee, bali alama ulizoacha kwenye roho za wengine.
Mbinu ya Tisa.
Nunua assets, badala ya liabilities.
Hii ndiyo kanuni kubwa zaidi inayotofautisha matajiri na maskini, wajasiriamali wakubwa na wale wanaojitahidi kila siku bila mafanikio. Matajiri hujua siri moja: nunua assets badala ya liabilities.
Asset ni kitu kinachoingiza pesa mfukoni mwako. Liabilities ni kitu kinachokutoa pesa mfukoni. Rahisi sana kusema, lakini watu wengi huchanganya. Wanafikiri gari kubwa ni asset, au simu ya kifahari ni asset, kumbe vyote hivyo vinawaongezea gharama za mafuta, matengenezo na matumizi yasiyo na kipato.
Kwa mfano, ukiamua kununua nyumba ya kupanga na ikawa inaleta kodi kila mwezi, hiyo ni asset. Lakini kama unanunua nyumba kubwa ya kuishi kwa mkopo bila mpango wa kuingiza kipato, hiyo ni liability, hata kama unaona ni fahari.
Unapotumia kipato chako, jiulize swali moja: hiki ninachonunua kitaleta pesa au kitanitoa pesa? Jibu la swali hili ndilo linaloweza kukutoa kwenye umasikini na kukupeleka kwenye uhuru wa kifedha.
Kila shilingi uliyopata ni mbegu. Ukiipanda kwenye assets, inakuletea mavuno ya kudumu. Ukiipoteza kwenye liabilities, inakunyima nafasi ya kujenga mustakabali wako. Matajiri hawana uchawi, wamejifunza tu kanuni hii na kuifanya sehemu ya maisha yao ya kila siku
Sasa hebu nikupe mtazamo mwingine wa nguvu zaidi:
Pafanye nyumbani kwako kuwa sehemu ya uwekezaji unaoleta faida. Iwe ni nyumba yako binafsi au hata umeamua kupanga, bado unaweza kuitumia kama chanzo cha kipato. Kama una nafasi, unaweza kutumia kwa kilimo cha bustani ndogo ndogo, hata kwa kutumia mifuko, madumu au makopo makuu. Unaweza kufuga kuku, samaki, sungura au hata nyuki kulingana na mazingira yako.
Ubunifu wako unaweza kubadilisha nyumba yako kuwa mradi mdogo wenye tija unaoongeza kipato kwa familia. Hata kama huwezi kufanya miradi mikubwa, unaweza kuanzisha mradi mdogo wa nyumbani na kuuendeleza hatua kwa hatua. Kila fursa iliyopo nyumbani kwako ni mtaji wa kuanzisha asset.
Kumbuka, kila pesa uliyopata ni mbegu. Ukiipanda kwenye assets, inakuletea mavuno ya kudumu. Ukiipoteza kwenye liabilities, unazidi kupoteza mustakabali wako. Hii ndiyo kanuni ambayo imejenga matajiri wengi kimyakimya.
Mbinu ya Kumi
Jiwekeze Wewe Mwenyewe
Watu wengi wanafikiri utajiri ni kupata pesa tu, lakini ukweli ni kuwa wewe ndiye rasilimali yako kubwa zaidi. Ukiwa na akili, mwili, na mtazamo imara, pesa zitakufuata kwa urahisi zaidi.
Jiwekeze kwa kujenga ujuzi unaohitajika, siyo kwa sababu unataka tu kujua, bali kwa sababu unataka kubadilisha maisha yako. Soma vitabu, jifunze biashara, lugha, au mbinu za kisayansi. Lakini usiishie kwenye somo, tafuta jinsi ya kutumia ujuzi huo kwenye hatua halisi ya maisha.
Hakikisha pia unajali afya yako na mtazamo wako wa akili. Mtu mwenye afya nzuri, akili imara, na moyo wenye mtazamo chanya, ana uwezo mkubwa wa kuunda fursa. Fanya mazoezi, chakula kizuri, pumziko la kutosha, na ujifunze kudhibiti hisia zako. Hii ni kuwekeza kwenye mtaji usioonekana, lakini wenye nguvu kuliko pesa yoyote.
Zaidi ya yote, jiwekeze kwenye tabia na nidhamu. Hizi ndizo zana ambazo zinakuweka mbele hata unapokabiliwa na dhoruba. Tabia ya kuanza mapema, kuweka akiba, kufanya maamuzi makini, na kushughulika na changamoto ni uwekezaji usio na kikomo.
Mwisho wa siku, uwekezaji huu unakuimarisha kufanya maamuzi sahihi, kuvunja vikwazo vya kifedha, na kukupeleka kwenye uhuru wa kweli. Kila pesa unayoingiza kwenye akiba au mradi ni nzuri, lakini uwekezaji kwenye wewe mwenyewe ndiyo msingi wa utajiri wa kudumu.
Asante kwa kufuatlia makala hizi. Nakutakia kila la heri katika kuyafanyia kazi yale uliyojifunza ambayo unaona yana msaada katika maendeleo yako ya kiuchumi, fedha na mafanikio kwa ujumla. Tukutane kwenye makala nyingine.
