Mbinu 10 za Kutoka Kwenye Umasikini (Sehemu ya 4)
Karibu mpenzi mfuatiliaji wa makala zetu. Hii ni sehemu ya nne katika mwendelezo wa makala ya Mbinu 10 za Kutoka kwenye Umasikini. Awali ya yote, kabla hujaendelea natamani uende ukasome sehemu ya kwanza, pili hadi ya 3 kwakuwa zimebeba msingi wa kuelewa sehemu hii ya 4.
Katika sehemu zilizopita, tulijifunza kuhusiana na dhana ya utajiri na umasikini na uhusiano wake na fikra za mwanadamu. Kwahiyo, utajiri ni matokeo! Kama ulivyo umasikini. Hiyo inatupa picha kwamba, mtu yeyote anaweza kubadilisha matokeo kwa kuelewa na kufuata kanuni ambazo zimethibitishwa na kutumiwa na watu wengi ambao wamefanikiwa.
Pamoja na hayo, tulijifunza mbinu kadhaa. Mbinu ya kwanza; Tafuta kuwa na kipato endelevu, Pili, Kuweka akiba. Tatu, Ishi chini ya kipato chako, nne, ongeza kipato chako. Leo tunajifunza mbinu ya tano ambayo ni kutumia taasisi za kifedha ili kukuwezesha kukua kwa haraka zaidi ya kudunduliza kipato chako kidogo kidogo.
Mbinu ya tano
Tumia Fedha za Watu Wengine!
Mbinu ya tano ya kutoka kwenye umasikini ni kutumia fedha za watu wengine. Watu wengi wanapofikiria kuhusu utajiri na mafanikio, akili yao huwapeleka moja kwa moja kwenye akiba ndogo ndogo wanazoweza kuweka kila mwezi kutokana na kipato chao. Ndiyo, hilo ni jambo jema na linajenga nidhamu ya kifedha, lakini ukweli mchungu ni kwamba njia hiyo ni ya polepole sana na mara nyingi huchelewesha sana safari yako ya kutoka kwenye umasikini. Ndiyo maana leo nakwambia wazi, ikiwa unataka kuondoka haraka kwenye hali ya kifedha inayokukandamiza, unatakiwa kujua namna ya kutumia fedha za watu wengine. Hii ndiyo siri ambayo wengi waliofanikiwa wanaitumia.
Unapokopa kutoka benki au taasisi za kifedha, au unapopata ufadhili wa ruzuku, au hata unapoingia ubia na mtu mwingine mwenye mitaji mikubwa, kile unachopata si tu pesa, bali ni leverage. Leverage ni nguvu inayokufanya usonge mbele kwa kasi kubwa zaidi kuliko ungeweza kutumia nguvu zako peke yako. Fikiria hili, kama una biashara ya kuuza bidhaa na unauza bidhaa 100 kwa mwezi kutokana na mtaji wako mdogo, lakini benki ikakukopesha fedha na ukaongeza mtaji wako mara tano, ghafla utaweza kuuza bidhaa 500 au zaidi. Faida unayoipata sasa inakuwa kubwa zaidi, na kwa muda mfupi unaanza kujiweka kwenye nafasi ya kutajirika haraka.
Watu wengi hushindwa kutumia mbinu hii kwa sababu ya hofu na kutojua. Wengine wanasema, “Kukopa ni kujitafutia matatizo.” Hii ni imani ya kizamani ambayo inakufanya ubaki pale pale. Ukweli ni kwamba ukikopa bila mpango, bila elimu, na bila mbinu za kisasa, ndiyo, unaweza kujiingiza kwenye shimo la madeni. Lakini ukikopa ukiwa na mpango thabiti, ukijua kabisa fedha hizi zinakwenda kuongeza biashara yako au mradi unaoeleweka, ukijua kabisa kuna mtiririko wa mapato utakaoirudisha hiyo fedha, basi mkopo unakuwa si mzigo bali ni ngazi ya kukupandisha juu ya umasikini.
Mfano wa watu wengi waliofanikiwa ulimwenguni ni kwamba waliwahi kukopa, waliwahi kutumia fedha za watu wengine, lakini walikuwa na mipango na nidhamu ya hali ya juu. Tajiri mkubwa kama Elon Musk aliwahi kuchukua mitaji ya wawekezaji wengine kuendeleza miradi yake, hata wajasiriamali wakubwa wa Tanzania na Afrika wametumia mitaji ya benki au washirika kufanikisha ndoto zao. Kwa nini wewe usitumie njia hiyo? Unapokaa chini na kuandika mpango wa biashara, unapojua namna mradi wako utakavyorudisha fedha, unapojifunza mbinu za kifedha, basi unakuwa umejipanga vizuri kutumia fedha za watu wengine kukutoa kwenye umasikini.
Wacha nikuulize swali, ni bora ukae miaka kumi na tano ukiweka akiba ndogo ndogo za shilingi elfu tano kila mwezi, au uchukue mkopo wenye masharti nafuu leo, ukawekeza kwenye mradi unaoleta faida na ukaanza kuona matunda ndani ya miezi michache? Watu waliofanikiwa hawakaa kungojea. Waliamua kuchukua hatua. Sasa jiulize, unasubiri nini?
Lakini kumbuka, nguvu ya kutumia fedha za watu wengine haipo tu kwenye kupata fedha, bali iko kwenye nidhamu, maarifa, na ujuzi wa kuzitumia fedha hizo kwa njia sahihi. Fedha ya mkopo siyo ya kula, siyo ya kuishi maisha ya anasa, bali ni chombo cha kukuondoa kwenye umasikini. Ni lazima uwe na maono, mipango ya kifedha, na uelewa wa biashara au uwekezaji unaoingia.Kama unataka kujifunza jinsi ya kukopesheka na taasisi za kifedha, kuna makala nimekuandalia. Unaweza kusoma kwa kubofya HAPA
Kwa hiyo, kama kweli una kiu ya kutoka kwenye umasikini, acha kuishi kwa hofu na fikra za kudunduliza peke yake. Fikiria nje ya boksi. Tafuta elimu ya kifedha, andaa mpango thabiti, tafuta taasisi zinazotoa mikopo kwa masharti nafuu, angalia uwezekano wa kuingia ubia na watu wenye mitaji, na tafuta fursa za ruzuku zinazopatikana ndani na nje ya nchi. Hapa ndipo unapoweza kujipatia fursa ya kweli ya kuondoka kwenye hali ya umasikini haraka.
Watu wanaposhangaa ni kwa nini wengine wamepiga hatua haraka kuliko wao, jibu mara nyingi ni kwamba hao waliopiga hatua waliamua kutumia fedha za watu wengine kwa busara. Ukijua jinsi ya kufanya hivyo, ukidhibiti tamaa, ukitumia fedha hizo kuongeza kipato na sio kuziua kwa matumizi yasiyo na maana, basi hakuna kitakachoweza kukuzuia kuondoka kwenye umasikini na kujenga maisha ya mafanikio.
Mwisho wa siku, kila kitu ni kuhusu uchaguzi. Utachagua kuendelea kudunduliza taratibu na kubaki hapo ulipo, au utachagua kutumia mbinu ya kutumia fedha za watu wengine kukupa nguvu ya kusogea mbele haraka? Uamuzi ni wako.
Tukutane sehemu ya tano
