Unaweza kuwa zaidi ya vile ulivyo
Unaweza kuwa zaidi. Hakuna kilicho kigumu wala kilichoganda juu yako. Mtu ulie leo si mwisho wa simulizi yako. Ni ukurasa tu, ni rasimu ambayo unaweza kuandika upya mara nyingi kadri utakavyoamua. Jana halina umiliki juu yako. Makosa yako hayakufafanui. Hata mafanikio ya jana si dari ya maisha yako. Wewe si bidhaa iliyokamilika, wewe ni mchakato.
Kila asubuhi unapoamka, maisha yanakukabidhi turubai jipya. Unachofikiria, unachoamua, unachofanya leo ndicho rangi inayopakwa humo. Wapo watakaokuambia kuwa binadamu habadiliki. Usikubali. Kila pumzi unayovuta ni ushahidi kwamba mabadiliko yanawezekana. Kukua si tukio, ni safari ya kuendelea kuwa.
Hatari si kushindwa. Hatari ni kuamini kwamba umekwama. Ukikubali uongo kwamba huwezi kubadilika, unajifunga kwenye gereza lenye mlango wazi. Ukweli ni kwamba unaweza kutoka wakati wowote. Unaweza kufikiri tofauti, kutenda tofauti, kuishi tofauti.
Kwa hiyo usijifunge kwenye simulizi ya jana. Usijinyime nafasi kwa kubaki kuwa picha ileile ya zamani. Simama leo na uanze upya. Amua kuwa zaidi. Kwa sababu hakuna kilicho kigumu, na kila kitu kinaweza kuandikwa upya.
